Kitaifa

Gazeti makini

Tuesday, November 5, 2013

Elimu ya Tanzania imekosa mkombozi

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
NA ELIZABETH HOMBO
NIMEKUWA nikitatizwa na mfumo wa elimu nchini, ingawa nami ni mmoja wa watu waliopitia kwenye mfumo huo, lakini ukweli ni kwamba umekuwa hauna tija kwa wananchi.

Mfumo wa elimu na sekta ya elimu kwa ujumla imetawaliwa na matatizo. Waathirika wakubwa kwenye suala hilo ni Mtanzania fukara mwenye kipato kisichoeleweka.

Kukosa kwake uwezo wa kumsomesha mtoto wake kwenye shule za gharama, kunamfanya kuendelea kukubaliana na uduni wa elimu nchini.

Matatizo kwenye elimu yamekithiri zaidi kwa walimu ambao hawathaminiwi.

Tumeshuhudia migomo mbalimbali ya walimu ambao wamekuwa wakidai haki na maslahi yao.

Hata hivyo migomo yao imekuwa ikizimwa kwa amri ya Mahakama Kitengo cha Kazi, wanalazimishwa kurejea kazini, jambo hilo linawafanya kuingiwa na ganzi ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Ni jambo gumu kwa mtu kukubali kuwajibika kikamilifu wakati hali yake kifedha si nzuri.

Mara kwa mara walimu wamekuwa wakigoma kufundisha kutokana na kutolipwa madai yao ya msingi.

Hata hivyo mara kadhaa Serikali imekuwa ikiahidi kutekeleza madai ya walimu.

Madai ya msingi ya walimu ni mengi, mathalani Serikali iliombwa kulipa madai hayo kwa asilimia 100, lakini ikashindwa na baadaye kuomba ilipe kwa asilimia 67. Hata hivyo Serikali haikufikia asilimia hizo na badala yake imekomea asilimia 24, hatua hiyo inawaweka walimu kwenye hali ngumu ya maisha na mwelekeo wa elimu nchini.

Kutokana na hilo, hakuna ubishi kwamba walimu wengi wanafundisha kwa mtindo wa bora liende, hawafundishi kwa moyo kama inavyotakiwa, wanafanya hivyo kwa sababu mioyo yao imetawaliwa na masononeko.

Pamoja na walimu kuwa na madai lukuki kama hayo, bado Serikali imekuwa ikija na mipango hafifu kwa kudai kuboresha mfumo wa elimu jambo ambalo halifanyiki.

Hata yale mabadiliko yanayofanyika hayawashirikishi kikamilifu wahusika ambao ni walimu.

Mabadiliko hayo yamekuwa yakifanywa na wanasiasa ambao mara nyingi wamekuwa wakiyaangalia matakwa yao ya kisiasa na si matakwa ya sekta husika.

Wanasiasa wamekuwa wakiweka mbele maslahi yao binafsi badala ya majukumu waliyopewa.

Wanashindwa kuwashirikisha wataalamu ambao wanafahamu nini cha kufanya ili kuwasaidia wananchi kuondokana na elimu duni.

Yapo masuala ya ajabu yanayofanywa na wanasiasa kama yale ya kubadili viwango vya matokeo.

Pengine haya yanatokea kwa sababu viongozi wakuu wa wizara pamoja na kuwa na taaluma ya ualimu, lakini wametawaliwa na siasa.

Kwa maana hiyo ni lazima watekeleze matakwa yao ya kisiasa kabla ya kugeukia matakwa ya nchi.

Hilo linasababisha kushuka kwa viwango vya ufaulu kila mwaka.

Tazama mchezo wa kisiasa ulivyokosa haya, walianza kwa kufuta matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, kisha wakatangaza matokeo mapya ambayo hayakuwa na nafuu yoyote.

Uamuzi huo ulifanywa kisiasa zaidi haukuwa na chembe ya utaalamu na utafiti juu ya kile wanachokifanya.

Baada ya tukio hilo sasa wamekuja tena na jipya kwa kubadilisha madaraja eti wamefuta daraja sifuri na anayepata daraja hilo atakuwa amefaulu kwa wastani wa daraja la tano, hata kama atakuwa amepata alama F kwenye masomo yote.

Ni wazi kwamba, hatua hii itazidisha kuzalisha wanafunzi mbumbumbu na bila shaka litakuwa ni taifa la ajabu kuwahi kutokea duniani.

Bado napata shida, inakuwaje mtu aliyepata sifuri aonekane amefaulu? Hawaoni kwa kufanya hivyo wanazidi kuwafanya wanafunzi wawe wavivu kusoma na kuendekeza mambo ya anasa badala ya kuzingatia masomo?

Kwa hali hiyo ni wazi wanafunzi wengi watapunguza moyo wa kujituma katika masomo yao kwa sababu wanajua hakuna kufeli kama ilivyokuwa awali, ambapo walijitahidi kusoma ili wasipate sifuri.

Hivi kweli katika maamuzi haya Serikali huwa inawashirikisha wadau wa elimu? Kutokana na haya ndio maana nahoji nani atakuja kuinusuru elimu ya Tanzania au ndio elimu yetu imekosa mkombozi? Je, tutegemee mkombozi kutoka nchi nyingine wakati jukumu hilo liko kwenye uwezo wetu.

Katika hali inayosikitisha Serikali inatangaza uamuzi huo huku matokeo ya mwaka jana yakionesha wanafunzi wakiandika majina ya wachezaji kama Lionel Messi na wengine wakichora michoro ya Zombi.

Katika muktadha huu Serikali inapoamua kuwabeba wanafunzi na kutangaza ufaulu mpya, unaleta maswali kuwa labda lengo la elimu yetu ni kujaribu kupata ufaulu badala ya kuikomboa nchi.

Kuanzia utawala wa Rais Mwinyi tuliona aliyekuwa Waziri wa Elimu, Jackson Makwetta akipendekeza mambo mbalimbali ambayo yangewezesha kuibadili elimu yetu.

Lakini kuanzia wakati huo tumezidi kushuhudia tume zilizoundwa pasipokuwa na majibu ya maana, kwani badala ya kuikomboa jamii zimekuwa zikijifurahisha na kuweka kabatini ripoti zote.

0 comments:

Post a Comment