Kitaifa

Gazeti makini

Tuesday, November 5, 2013

Taswira ya Tanzania kiuwekezaji yadorora

Taswira ya Tanzania kiuwekezaji yadorora
*Rushwa, miundombinu, umeme vyaiponza
*Yashika nafasi ya 145 kati ya mataifa 189
*Nyota ya Rwanda yang’ara kimataif
a

Na Gabriel Mushi
TASWIRA ya Tanzania katika ubora wa mazingira ya kiuwekezaji na kwa kuwa na fursa zinazovutia biashara kimataifa imeendelea kuporomoka, Rai Jumatano limebaini.

Ripoti mbili za kimataifa zilizotolewa na taasisi mbili za kiuchumi na kibiashara zinazoheshimika, Benki ya Dunia na ile ya Kongamano la Biashara la Dunia zote zinatoa taswira hiyo ya mdororo ambao umewashtua baadhi ya wadadisi wa masuala ya uchumi na uwekezaji.

Dodoso la kwanza linaloiweka Tanzania katika sura hiyo ya mporomoko limo katika ripoti ya ‘The Global Competitiveness Report 2013–2014 (Ripoti ya Ushindani ya Dunia ya mwaka 2013 – 2014).

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba, Tanzania inashika nafasi ya 125 duniani kwa kuwa na taasisi zinazovutia mazingira ya kiushindani kibiashara miongoni mwa mataifa 128, jambo ambalo ni mporomoko wa hatua tatu kutoka nafasi ya 120 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita iliposhika nafasi ya 120.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inaeleza kwamba, mporomoko huo unachangiwa kwa kiwango kikubwa na kuzorota kwa mambo katika maeneo kadhaa yakiwamo yale ya taratibu za kisheria na kimaadili.

Ripoti hiyo inaainisha kwamba katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, kumekuwa na kushamiri kwa vitendo vya rushwa kulinganisha na miaka iliyopita sambamba na kudorora kwa uwazi katika masuala yanayohusu uandaaji wa sera.

Mbali ya hayo, miongoni mwa mambo yanayotajwa kuathiri taswira ya ushindani wa Tanzania kibiashara ni ubovu au uhafifu wa miundombinu kama barabara, kukosekana kwa umeme wa uhakika na huduma zisizoridhisha za bandari.

“Kwa upande mwingine miundombinu ya Tanzania bado ni duni huku huduma za barabara na bandari zikiwa hafifu na kukosekana kwa uhakika kwa nishati ya umeme,” ilisema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaonyesha Tanzania inashika nafasi ya 106 kwa kuwa na matendo mengi ya rushwa, ya 134 kwa kuwa na miundombinu duni na nafasi ya 131 kwa kukosekana kwa umeme wa uhakika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ingawa Tanzania inaonekana kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na elimu yua msingi inatajwa kuwa miongoni mwa mataifa yenye idadi ndogo zaidi duniani kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondani na vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa viwango vilivyoainishwa katika ripoti hiyo, Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya 134 kwa kuwa na idadi ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari huku ikishika nafasi ya 138 kwa wale wanaopata elimu ya vyuo vikuu.

Kama hiyo haitoshi, ripoti hiyo pia inaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye fursa duni kwa upande wa maendeleo ya teknolojia ya kompyuta (Tehama) na ya simu za mikononi ikiwa nafasi ya 126 miongoni mwa mataifa 148.

Kwa upande wa Ripoti ya Benki ya Dunia (Doing Business Report 2014) imeonesha kuwa Tanzania imeendelea kuporomoka kwa nafasi tisa kutoka nafasi ya 136 mwaka 2012 hadi nafasi ya 145 mwaka huu kwa kuwa na mazingira mepesi yanayovutia biashara.

Uchambuzi wa ripoti hiyo inaonyesha kwamba, kabla ya kufikia hatua hiyo mwaka huu, miaka miwili tu iliyopita (2011) Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 128 kabla ya kuporomoka zaidi kwa nafasi nane katika kipindi cha mwaka mmoja tu na baadaye kwa nafasi 19.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyojumuisha nchi 189 ulimwenguni na kuwekwa hadharani Oktoba 29, mwaka huu, taifa dogo la Rwanda linaonekana kuwa kinara kwa kushika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki na miongoni mwa mataifa yenye uchumi mdogo duniani.

Katika ripoti hiyo pia Tanzania imetajwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa na urasimu katika maeneo ya upatikanaji wa huduma muhimu, ambazo kwenye nchi nyingine zinapatikana kwa urahisi.

Maeneo yaliyoanishwa na ripoti hiyo ni kama vile upatikanaji wa kibali cha ujenzi wa nyumba ( nafasi ya 177 kati ya nchi 189), hati ya kumiliki nyumba (nafasi ya 146 kati ya nchi 189) na usumbufu kwenye ulipaji wa kodi (nafasi ya 177 kati ya nchi 189).

Katika maeneo mengine, ripoti hiyo inaonyesha kwa upande wa ugumu wa kupata mikopo (nafasi ya 130 kati ya nchi 189), ugumu wa kusajili na kupata leseni ya biashara (nafasi ya 119 kati ya nchi 189), na ugumu wa kupata nishati ya umeme (nafasi ya 102 kati ya nchi 189).

Akizungumzia ripoti hiyo mwanasiasa na mchumi wa kimataifa, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema hali hiyo inajitokeza kutokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa na uongozi wenye dira madhubuti ya kufanya biashara na kuongeza ajira.

Profesa Lipumba alieleza kukubaliana na ripoti zote hizo mbili ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya World Economic Forum (WEF).

“Tanzania iko chini sana katika ushindani wa kiuchumi kwa sababu asasi zake za kiuchumi ni dhaifu na hazifanyi kazi kwa ufanisi, rushwa na ufisadi unazidi kuongezeka, na maumuzi ya sera hayako wazi na siyo thabiti.

“Mameneja wa kampuni kubwa zinazofanya biashara Tanzania wameeleza kuwa matatizo makubwa ya shughuli za kiuchumi Tanzania ni pamoja na ukosefu wa mikopo, rushwa na ufisadi, miundombinu mibovu, utendaji mbovu na urasimu wa watumishi wa serikali na mfumko wa bei,” alisema.

Alifafanua kuwa ili kupima ushindani wa kiuchumi wa kila nchi, watafiti wamechunguza mambo ya msingi yanayochochea ukuaji wa uchumi na uletaji wa maendeleo kwa ujumla.

Alisema ili Tanzania iweze kushindana na kunufaika katika ulimwengu wa utandawazi inahitaji iwekeze katika miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, ufuaji na usambazaji wa umeme, miundombinu ya maji safi na maji taka TEHAMA na kuboresha elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honesty Ngowi, alisema hilo ni pigo kwa serikali kwa sababu juhudi zinazooneshwa na serikali katika kuvutia uwekezaji nchini zimegonga mwamba.

“Suala la rushwa, na urasimu ndio chanzo cha haya yote kwa sabahu tunaona kuwa tangu mwaka 1960 hadi miaka ya 1980, serikali ilikuwa ikijipanga kuweka mikakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji, lakini cha ajabu hadi kufikia sasa ndio kwanza tunazidi kushuka.

“Tunatakiwa kujitathmini tumekosea wapi, na namna gani ya kuondokana na matatizo haya kwani hata katika awamu hii suala la kuvutia wawekezaji limekuwa likipigiwa debe sana, lakini hakuna kitu tunazidi kushuka,” alisema

Anguko hilo la Tanzania kiuchumi limekuja katika kipindi ambacho serikali ya awamu ya nne iko katika mikakati kadhaa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji nchini.s

Benki ya Dunia imekuwa na taratibu za kutoa ripoti ya mazingira ya kufanya biashara katika nchi zote duniani kila mwaka.

Wakati Tanzania ikiporomoka kwa nafasi tisa nchi jirani ya Rwanda iliyokuwa na hali ngumu ya kufanya biashara, imefanikiwa kurekebisha mazingira ya biashara na kushika nafasi 32 kati ya nchi 189.

Ikumbukwe kuwa mwaka jana Rwanda ilikuwa ya 54 kwa hali hiyo nchi hiyo inayoongozwa na Rais Paul Kagame imepanda juu kwa nafasi 22.

Nchi zinazoongoza kwa ushindani wa kiuchumi wa mataifa ni Uswissi, ikifuatiwa na Singapore, Finland, Ujerumani, Marekani, Swiden, Hongkong, Uholanzi (Netherlands), Japan na Uingereza

Katika nchi za Afrika, inayoongoza kwa ushindani wa kiuchumi ni Mauritius inayoshika namba ya 45, ikifuatiwa na Afrika Kusini ambayo ni ya 53 na ya tatu ni Rwanda iliyoshika nafasi ya 66 katika orodha ya nchi 148.

Mauritius imeipiku Afrika Kusini iliyokuwa inaongoza mwaka jana.

0 comments:

Post a Comment