Kitaifa

Gazeti makini

Sunday, November 10, 2013

Lowassa: Nasikitishwa elimu duni shule za kata

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
WAZIRI Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amesikitishwa na kiwango duni cha elimu katika shule za sekondari za kata na baadhi ya vyuo vya elimu ya juu.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia mfuko wa elimu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, alisema kiwango cha elimu katika shule hizo kinamsikitisha kwa kuwa ni cha chini.

“Napenda niseme wazi kuwa kiwango cha elimu katika shule za kata na baadhi ya vyuo vikuu, kwa kweli ni vya chini, hili mimi linanisikitisha sana kwa sababu elimu bora ni mkombozi kwa mtoto wa Kitanzania,” alisema Lowassa.

Alipongeza kanisa kwa kusaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha na kuboresha elimu, ambapo shule nyingi za kanisa zimekuwa na kiwango cha juu cha elimu.

Alitumia nafasi hiyo kuonyesha misuli yake kisiasa na kijamii ambayo ni marafiki wanaomsindikiza katika harambee mbalimbali.

“Sasa napenda Watanzania kupitia kwenu kuwaonyesha hawa marafiki zangu ambao wamekuwa wananisindikiza katika harambee, maana kumekuwa na maneno maneno,” alisema Lowassa baada ya wakili maarufu, Sadock Magai kuwasilisha michango ya marafiki.

Marafiki wa Lowassa walichangia Sh milioni 50 ambao ni Lawrence Masha, Innocent Macha, Bashir Awale, Hamis Kindoroko na Lemmy Bathelemew.

Aidha, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, alichangia Sh milioni tatu na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azan, alichangia Sh milioni mbili.

“Nampongeza na kumshukuru Idd Azan kwa kuja kwake kunisindikiza na kuchangia, hii ndiyo Tanzania ninayoijua, isiyo na dini, watu wa dini zote mnashirikiana,” alisema Lowassa.

Katika harambee hiyo, jumla ya Sh milioni 615 zikiwa ni fedha taslimu pamoja na ahadi zilipatikana na kuvuka lengo ambalo lilikuwa ni Sh milioni 250.

0 comments:

Post a Comment