Kitaifa

Gazeti makini

Tuesday, November 5, 2013

Kujiuzulu ni uadilifu wa kukiri upungufu

MTU anapokubali nafasi ya uongozi, maana yake ni kwamba anakubali kubeba wajibu mzima kuhusiana na ufanisi wa majukumu yake mahali pale anapopaongoza.

Kwa bahati mbaya sana, viongozi wetu nchini ni wepesi wa kupokea sifa kutokana na utendaji mzuri wa wale walio chini yao. Lakini mambo yanapokwenda vibaya, viongozi hao hao ndio huwa wa kwanza kujiweka mbali na makosa yaliyotendeka.

Tunasema kuwa kimsingi “kujiuzulu” si sawa na “kukiri kosa” moja kwa moja kwamba umelitenda.

 Kinyume chake, kujiuzulu ni tabia ya uadilifu, ambapo mhusika anakiri upungufu wake katika kusimamia majukumu yake.

Katika nchi zilizoendelea, ambazo tunapenda kuiga mienendo yao, kujiuzulu ni dhana ya uungwana na uadilifu. Viongozi hujiuzulu kazi zao inapodaiwa au wanapojihisi wao wenyewe kuwa wameshindwa kusimamia majukumu yao kama inavyopasa.

Aidha, hujiuzulu wao wenyewe bila shinikizo kutoka mahali popote baada ya kuzingirwa na kashfa, ama wao binafsi kama wao au sehemu wanazoziongoza kushindwa kuonyesha ufanisi na matarajio ya wale waliowapa dhamana.

Kwa Tanzania, hili jambo limekuwa gumu mno kwa viongozi kulielewa. Hawataki kujiuzulu hata mahali ambapo makosa yao yanaonekana dhahiri!

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kujiuzulu akiwa waziri baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani aliyokuwa akiiongoza kukumbwa na kashfa, lakini uamuzi wake huo haukumzuia kuwa Rais.

Huko nyuma wananchi, wakiwamo baadhi ya viongozi na wabunge, mara kadhaa walimtaka aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, William Ngeleja, kujiuzulu kwa kushindwa kufikia matarajio ya Watanzania ya kuwapatia umeme wa uhakika.

Yeye aliwajibu kuwa hatajiuzulu ng’o, na kweli hakujiuzulu hadi mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yalipofanyika.

Ngeleja hayuko peke yake. Yumo aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami na aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu akisimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika.

Wapo wengine, wakiwamo wakuu wa taasisi, ambao walitajwa na wamekuwa wakiendelea kutajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba wanahusika katika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Huu ndio utamaduni wa viongozi wa Kitanzania, kwa maana kwamba kiongozi hatoki madarakani hadi apigwe mawe.

Hivi karibuni baada ya matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne, ambayo yalisababisha baadhi ya wanafunzi kujiua, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, naye kwa jeuri kubwa aliwaambia Watanzania kuwa hatajiuzulu.

Kisa? Eti kwani akijiuzulu kitendo hicho kitaboresha elimu nchini! Maneno yake hayo ya kujiamini, aliyasema bila woga wala aibu.

Wiki iliyopita mjini Dodoma, wabunge walichachamaa wakiwataka wabunge watano, akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wajiuzulu kwa kushindwa kusimamia vizuri Operesheni Tokomeza Ujangili na kutatua migogoro ya wafugaji, wamegoma.

Tunasema kuwa mawaziri hawa wasingoje matokeo ya Tume ya Bunge, wapime wenyewe. Wakiona wanalazimika kubeba wajibu, wafanye hivyo.

Hii ndiyo tabia ya uadilifu kwa kiongozi.

0 comments:

Post a Comment